"NDANI ya chumba cha uendeshaji wa mitambo, tulikuwa kama wataalamu 16. Mimi nilitoka nje kuongea na simu, vinginevyo ningekuwa miongoni mwa waliopoteza maisha.
“Pia meneja mkuu wa kiwanda naye alitoka muda huo kwenda kwenye boiler (mtambo wa kuchemshia) kukagua shughuli zinazoendelea kama ziko sawa.”
Hiyo ni kauli ya Meneja wa Kitengo cha Umeme na Vifaa wa Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa, Juma Palamba, alipozungumza na mwandishi wa Habari hii akielezea tukio la mlipuko uliotokea katika chumba maalum cha uendeshaji wa mitambo na kusababisha vifo vya watu 11 na mmoja kujeruhiwa.
Waliofariki dunia katika tukio hilo ni raia watatu wa kigeni kutoka Brazil, Kenya na India na Watanzania wawili ambao walijeruhiwa wakati wakifanya majaribio ya mtambo wa mvuke uliokuwa umeboreshwa kwa kuongezewa nguvu ya uendeshaji.
Alisema tukio hilo lilitokea Mei 23, mwaka huu, katika kiwanda hicho kilichoko Turiani, Mvomero mkoani Morogoro.
Palamba alisema akiwa anaongea na simu, alimwona msaidizi wake mwingine akiwa nje pia anaongea na simu na kwamba wao na wenzao ambao ni meneja uzalishaji ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya meneja wa kiwanda walinusurika.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo, ni opereta na msaidizi wake ambao walikuwa ndani lakini inaonekana mvuke haukuwapiga moja kwa moja kama wengine waliofariki dunia.
Palamba alisema hitilafu hiyo imetokea wakati wa majaribio ya mitambo iliyoongezwa uwezo na walikuwa katika hatua ya mwisho ya majaribio ili leo kuanza rasmi msimu mpya wa uzalishaji.
"Ni ajali ambayo imetokea baada ya ‘pipe’ (bomba) ambayo inapokea ‘steam’ (mvuke) kupeleka kwenye mtambo wa kuchemshia inayotoa fito 45 na kipimo cha nyuzi joto inafikia hadi 450.
“Tukio lilivyotokea ni kwamba walishazalisha mvuke, wakaufungulia kuupeleka eneo la kuzalisha umeme. Lengo kubwa lilikuwa kufanya majaribio baada ya kuongezea nguvu injini ya mvuke, maji na gesi yetu ambayo mwanzo ilikuwa ikitumia mvuke wa fiyo (bar) 24 na nyuzi joto 300," alisema.
Pia alisema katika kuboresha mifumo huwa kuna mabadiliko mbalimbali yanafanyika kabla ya kuwezesha mtambo wa kuchemshia kuhimili kupokea na kutoa mvuke kwa kiwango kikubwa zaidi sambamba na kupima kama injini itahimili mabadiliko husika ndiyo maana jaribio la kwanza lilikuwa kuiongezea nguvu njia iwe na uwezo wa kupokea ‘bar’ 45.
Alisema jaribio la pili lilikuwa la kubadilisha mabomba ya kusafirishia mvuke kwa sababu kuna sehemu ambazo mabomba yalikuwa na uwezo wa kupokea fito 24 tu, hivyo kazi ya kubadilisha ilifanyika.
"Leo (jana) sasa baada ya kufanya majaribio ili kesho (leo) tuanze uzalishaji rasmi, ndipo hiyo hitilafu ikatokea. Bahati mbaya sasa mvuke ulipokewa kabla ya kufikia kuzungusha mtambo wa mvuke.
“Wakati tukisubiri mvuke na nyuzi joto vipande ili kuruhusu mtambo kuwashwa, wakagundua katika hayo mabomba yaliyobadilishwa ambayo pia yana maeneo ya maungio yanayoruhusu kutanuka na kusinyaa, baada ya kupokea bar 45, pakaonekana sehemu moja ni dhaifu na pakachanika, hivyo kusababisha mvuke wote uliokuwa ukitokea eneo la kuchemshia kutoka nje," alisema.
Alisema mvuke huo wote uliokuwa ukisafirishwa kwa mwendokasi wa kati ya 30 hadi 45 kwa nyuzi joto 450, wote ulikwenda kwenye chumba cha kuendesha mitambo ambako waendesha mitambo, yaani maopereta na wataalam wengine, akiwemo mtengenezaji wa mtambo wa mvuke, wataalamu wa kutoka vitengo mbalimbali na wasaidizi wao wote walikuwa wakiangalia majaribio, ili kila mmoja aifanyie kazi eneo lake.
Kwa mujibu wa mtaalam huyo, miongoni mwa watu 11 waliofariki dunia ni pamoja na mtengenezaji na mwendeshaji wa mtambo huo wa mvuke raia wa Brazil, mhandisi mwingine raia wa Kenya ambaye ni msaidizi wake katika kitengo cha umeme, mhandisi mwingine raia wa India na wataalamu wanane, raia wa Tanzania.
KAMANDA ATHIBITISHA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP) Alex Mkama, aliyefika eneo la tukio, alisema hitilafu hiyo ya umeme ilitokea kwenye mtambo wa kupitisha mvuke wa kuzalisha umeme kiwandani hapo.
Mkama alisema majeruhi wawili wa ajali hiyo, akiwamo Mtanzania mmoja na raia mwingine wa kigeni (majina bado) wamepelekwa Hospitali ya Misheni ya Bwagala kwa matibabu zaidi
TANESCO, ZIMAMOTO
Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro Shaban Marugujo, alisema: "Kilichotokea ni bomba la mvuke kutoka boiler namba 4 kwenda chumba cha kuzalisha umeme lenye uwezo wa kubeba bar 45 kwenye maungio yake lilishindwa kuhimili, hivyo kuachia na kwenda kupiga kwenye chumba cha mawasiliano walikuwako watu na kufariki dunia papo hapo."
Alisema hadi sasa chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika na uchunguzi zaidi wa tukio hilo bado unaendelea kwa kushirikisha wataalam mbalimbali.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Turiani, Dk. David Ruchwanisa, alisema usiku wa kuamkia Mei 23, majira ya saa 10:00 usiku walipokea majeruhi wawili wa jinsia ya kiume na waliwapatia matibabu na baadaye kupewa rufani kwenda Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dodoma kwa matibabu zaidi kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Alisema majeruhi hao wameungua maeneo mbalimbali ya miili yao ikiwemo tumboni, kifuani miguuni na mikononi.
Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Morogoro Mhandisi Fadhili Chilombe, alisema mfumo huo ulikuwa unatumia umeme kidogo wakati wa kuwasha na badaye kujiendesha wenyewe.
Alisema kutokana na mlipuko huo kwa sasa hautaweza kujiendesha na kwamba pale watakapohitaji huduma ya umeme, TANESCO wako tayari kuwahudumia ili shughuli za kiwanda zisisimame.