Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mwl. Linno Mwageni amewataka Wanafunzi wanao shiriki mashindano ya michezo kwa shule za Msingi – UMITASHUMTA Wilayani Mvomero kuwa na nidhamu ili waweze kupata mafanikio katika mashindano hayo.
Mwl. Mwageni ametoa wito huo leo Mei 26, 2024 wakati akifungua mashindano ya UMITASHUMTA kwa ngazi ya Wilaya ambayo yanaendelea katika viwanja vya michezo vya Chuo Kikuu Mzumbe .
Mkurugenzi huyo amesema nidhamu na bidii humfanya mtu kuyafikia malengo yake ambayo amejiwekea hivyo akawasisitiza washiriki hao ili waweze kufika mbali katika sekta ya michezo.
“...jamani mkishindwa kuleta vikombe vyote mkaniletee kikombe cha nidhamu kwa sababu hicho hakihitaji kuvuja jasho wala nini kinachotakiwa kila kitu mfanye kwa nidhamu...” amesema Mwl. Mwageni.
Aidha amewataka washiriki kujituma katika mashindano hayo na kwamba wasiende kushiriki bali wakashindane ili wapate nafasi katika ngazi zote kuanzia ya Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Mwl. Mwageni amewashukuru na kuwapongeza walimu ambao wamewatoa wanafunzi wao ili washiriki UMITASHUMTA huku akiwataka kuwa walezi bora wa wanafunzi hao.
Kwa upande wake Afisa michezo wa Halmashauri hiyo Bw. Charles Kajiru amebainisha kuwa kambi hiyo ni ya siku tatu kuanzia leo Mei 26 hadi Mei 28 na michezo inayoshindanishwa ni pamoja na mpira wa miguu, mikono, wavu, kikapu, mpira wa pete na kwaya. Ameongeza kuwa timu ya Wilaya itakuwa na wachezaji 88 hadi 90, walimu 10 pamoja na viongozi wengine.
Nao washiriki wa michezo hiyo akiwemo Thomas Ventus amesema timu yao ya mpira wa wavu ilifanya vizuri katika mashindano ya UMITASHUMTA 2023 na kwamba anaamini na mwaka huu watafanya vizuri zaidi.
Mashindano ya UMITASHUMTA 2024 yanaenda sambamba na kaulimbiu isemayo “Miaka 50 ya UMITASHUMTA, Tunajivunia mafanikio katika Sekta ya Elimu, Michezo na Sanaa, hima mtanzania shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024”