Mhe. Nguli amebainisha hayo Mei 16 mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Njeule kwenye mkutano wa hadhara ikiwa ni ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi Wilayani humo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema pamoja na kusoma taarifa zinazohusu mgogoro huo na kusikiliza wananchi ameunda timu ya wataalam ambao watafika kijijini hapo kwa ajili kuchunguza mgogoro huo kwa kufanya mahojiano na wananchi, mmiliki wa shamba hilo na viongozi wa Kijiji hicho, timu hiyo imepewa siku 14 kufanya uchunguzi huku akisema kuwa majibu ya ripoti hiyo itatolewa baada ya siku 21.
“...waliouza na waliouziwa wote watahojiwa na Afisa ardhi atatoa timu na mimi nitatoa timu ya maafisa watakuja hapa...ndani ya siku 14 kuanzia leo nitapewa hiyo ripoti...” amesema Mkuu wa Wilaya.
Mhe. Nguli amewataka wananchi kusitisha shughuli za kilimo katika eneo hilo lenye mgogoro isipokuwa kwa shughuli ya uvunaji pekee wakati timu hiyo ikiendelea na uchunguzi. Aidha amewataadharisha wananchi dhidi ya watu watakao tumia mgogoro huo kwa maslahi ya kisiasa na kuwataka wananchi kuwakwepa watu hao.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika mwaka huu.
Sambamba na hilo Mhe. Nguli ameahidi kuzifanyia kazi kero zilizoibiliwa na wananchi ili ziweze kutatuliwa.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lukwemzi Mhe. Zakaria Benjamini ameeleza kero ya kukosekana kwa shule ya msingi hali inayosababisha wanafunzi kutembea umbali wa kilometa 14 kwa ajili ya kupata elimu katika Kijiji cha Njeula hivyo ameiomba Serikali kusaidia umaliziaji wa vyumba viwili vya madarasa ambavyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi ambapo ujenzi huo umefikia hatua ya lenta.