Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Judith Nguli amewataka wadau wa kilimo Wilayani humo kuupokea kwa mikono miwili Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa kuwa mfumo huo utawainua wakulima na kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo.
Mhe. Nguli ametoa wito huo Mei 16, 2024 wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Mfumo wa stakabadhi za ghala ili kuuza mazao ya Ufuta, Mbaazi, Alizeti na Korosho uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mvomero.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema wakulima wamekuwa hawapati faida kutokana na kuuza mazao yao kwa mifumo isiyo rasmi hali hiyo inasababisha Halmashauri kushindwa kukusanya mapato yake halisi, hivyo amewataka Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa Kata, Maafisa kilimo pamoja na wakulima kuukubali mfumo huo ili kuinua hali za wakulima na mapato ya Halmashauri.
“...Mvomero tuna ardhi nzuri, inarutuba, inazalisha na inatija tukitumia huu mfumo vizuri matokeo yake kwa wakulima wetu ni makubwa...” amesema Mhe. Judith Nguli.
Aidha, ameongeza kuwa mfumo huo unafaida kwa wakulima kwa kuwa utawahakikishia upatikanaji wa masoko, usalama wa mazao yao, utawaepusha na madalali ambao wamekuwa wakinunua mazao kwa bei ya chini, wakulima watakutanishwa na taasisi za kifedha na kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao wanayolima.
Katika hatua nyingine, Mhe. Judith Nguli amewataka wakulima Wilayani humo kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili kuwawezesha kuuza mazao yao na kupata pembejeo za kilimo kwa urahisi.
Sambamba na hilo, amewataka Viongozi wa kisiasa Wilayani humo kutoa elimu na kuhamasisha wakulima katika maeneo yao kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani wakati wa kuuza mazao yao.
Awali wakati akisoma taarifa ya hali ya uzalishaji wa mazao ya kilimo Wilayani humo, Afisa Kilimo wa Halmshauri ya Wilaya ya Mvomero Bi. Ruth Mazengo amesema Halmashauri imepoteza mapato kiasi cha shilingi 5,000,337,878 kutokana na wakulima kuuza mazao ya Ufuta, Alizeti, Mbaazi na Korosho kwa mfumo usiyo rasmi.
Aidha, Bi. Ruth ameeleza faida zitakazopatikana ikiwa wakulima watauza mazao yao kwa mfumo wa Stakabadhi Ghalani ni Pamoja na mazao yatauzwa kwa bei halisi hivyo kuisaidia Halmashauri kupata mapato yake, upatikanaji wa masoko ya uhakika na usalama wa mazao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mhe. Yusuph Makunja amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuwa na nia ya dhati ya kuinua Halmashauri kutoka mahali ilipo sasa. Pia amemuhakikishia kuwa Waheshimiwa Madiwani wataupokea mfumo huo kwa manufaa ya Halmashauri na wakulima ambao ndiyo wa piga kura wao.