Wilaya ya Mvomero imepanga kuanza mchakato wa kukagua utendaji kazi wa mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs) yanayofanya kazi katika Wilaya hiyo ili kuhakikisha kuwa yanafuata kanuni, sheria na malengo yaliyokusudiwa kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa Novemba Mosi mwaka huu na KatibuTawala wa Wilaya ya Mvomero, Bw. Saidi Nguya wakati akifungua Kikao kazi cha Mashirika yasiyo ya Kiserikali ngazi ya Wilaya kwa Robo ya Kwanza kipindi cha Julai - Septemba 2024 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Katibu Tawala huyo amesema mchakato huo unalenga kutathmini na kubaini kama mashirika haya yanatimiza malengo na ahadi walizoweka kupitia maandiko yao kwa jamii na wafadhili wao huku akisisitiza kuwa ni muhimu mashirika haya kufuata miongozo iliyowekwa ili kuimarisha uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Mvomero.
"...kama ambavyo tunaikagua miradi ya Ruwasa, tunaikagua miradi ya barabara, tunakagua miradi ya shule, miradi ya hospitali, tunataka kuanze kufanya ufuatiliaji wa taasisi baada ya taasisi, shirika kwa shirika..." amesisitiza Katibu Tawala.
Aidha, ameongeza kuwa kupitia ukaguzi huu, watajiridhisha kama mashirika haya yanafanya kazi kwa uwazi na uadilifu, na kwamba rasilimali wanazotumia zinawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa huku akibainisha kuwa baada ya ukaguzi huo taarifa itatolewa itakayoainisha mashirika ambayo yanatekeleza kwa vitendo maandiko ya miradi yao kwa wananchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mwl. Linno Mwageni ameyataka mashirika hayo kutekeleza majukumu yao kwa kufuata mila na desturi za nchi ya Tanzania na kuacha kuiga tamaduni za kigeni ambazo ni kinyume maadili ya mtanzania.
Awali wakati akisoma taarifa ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Mratibu wa Mashirika hayo Wilaya ya Mvomero Bw. Azizi Msuya amesema katika Wilaya hiyo ina Mashirika 60 ambayo yanafanya kazi, Bw. Msuya ameongeza kuwa Mashirika hayo yanatekeleza miradi mbalimbali katika Sekta za Elimu, Sheria, Kilimo, Mifugo, Afya pamoja na mazingira.